Bamba la gandunia

Mabamba gandunia ya dunia yetu.

Bamba gandunia ni jina lililobuniwa hivi karibuni[1] kwa mapande yanayounda sehemu ya nje ya dunia yetu. Sehemu hiyo ya nje huitwa ganda la dunia na chini yake kuna sehemu ya dunia ambayo ni ya joto kiasi ya kwamba miamba na elementi zote zinapatikana katika hali ya giligili yaani kuyeyushwa. Hiyo sehemu ya nje ya dunia si pande moja bali kuna mapande mbalimbali kandokando yanayoelea juu ya mata ya moto ndani yake. Unaweza kusoma zaidi katika makala kuhusu muundo wa dunia.

Gandunia ni elimu kuhusu ganda la dunia. Hoja ya sayansi kuhusu gandunia ni kwamba ganda la dunia limevunjika mapandemapande yanayoitwa mabamba. Kila bamba linapakana na mabamba mengine. Mabamba yasukumwa na mikondo ya moto chini yake kama majani yanayokaa usoni mwa maji yanayoanza kuchemka katika sufuria. Hivyo kila bamba lina mwendo wake wa pekee pamoja na au dhidi ya mabamba mengine. Tetemeko la ardhi ni dalili ya kwamba mabamba yamesuguana na hivyo kusababisha mishtuko tunayojua kama tetemeko la ardhi.

Mabamba hayo ni sehemu ya nje ya tabakamwamba (lithosferi). Tabaka hilo limevunjika katika mapande makubwa 7 na vingine vidogo vinavyoelea juu ya tabaka lenye hali ya kiowevu chenye mnato mzito.

Mabamba hayo yote yameonekana kuwa na mwendo wa sentimita kadhaa (cm 2 - 20 zimepimwa) kwa mwaka. Mwendo huo husababishwa na nguvu ya magma (mwamba moto wa kiowevu) inayopanda juu na kusukuma mabamba hayo.

  1. Neno gandunia si kawaida bado, tunafuata hapo kamusi ya KAST.

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Tubidy