Ukanamungu

Profesa Richard Dawkins ni mwatheisti mashuhuri wa karne ya 21.

Ukanamungu (pia: Uatheisti kutoka neno la Kiyunani cha kale, atheos, likiwa na maana ya "bila miungu") kijumla ni msimamo wa kutokuwa na imani juu wa uwepo wa miungu, ama kukataa imani kuwa kuna miungu, yaani ni dhana kuwa hakuna Mungu wala miungu. Hivyo ni kinyume cha Utheisti, imani kuwa angalau kuna Mungu mmoja.

Asili ya neno Uatheisti, limechipuka hata kabla ya karne ya 5, lilitumika kuwakilisha wale wasioamini uwepo wa miungu inayoabudiwa na jamii kubwa ya watu, wale waliovunjwa mioyo na miungu, au wale wasioona sababu yoyote ya msingi ya kuamini uwepo wa miungu.

Neno lenyewe uatheisti lilianza kutumika hasa mnamo karne ya 16, baada ya kusambaa kwa fikra huru dhidi ya dini.

Watu wa kwanza kujitambulisha kama waatheisti, waliishi karne ya 18 wakati wa Zama za Mwangaza; mapinduzi ya Ufaransa yalishuhudia vuguvugu kubwa la kisiasa kuwahi kutokea kwenye historia, lililotetea ukuu wa fikra za binadamu.

Hoja zinazotetea uatheisti, zimegawanyika kwenye makundi mbalimbali yakiwemo ya kifalsafa, kijamii na kihistoria.

Mantiki ya kutoamini uwepo wa miungu inajumuisha, tatizo la uovu, hoja ya funuo zinazokinzana, na kukataa dhana isiyoweza kupingika.

Wasioamini wanadai kuwa uatheisti ndio dhana asili ya binadamu kuliko Utheisti, kwa sababu kila mtu anazaliwa bila kuwa na imani ya Mungu au miungu; kwa maana hiyo basi, ni jukumu la anayeamini uwepo wa miungu au Mungu kuthibitisha madai yake na si jukumu la atheisti kuthibitisha kuwa hakuna Mungu au miungu.

Tafiti za zamani kutoka shirika la habari la Uingereza (BBC), zilionyesha kuwa 8% ya watu wote duniani ni waatheisti, huku zile za zamani zaidi zikionyesha kuwa ni 2% pekee, na wale wasiokuwa na dini yoyote wakiunda 12% ya watu wote duniani.

Mwaka 2015, tafiti zimeonyesha 61% ya watu wa China walikuwa waatheisti, huku tafiti za mwaka 2010 zikionyesha kuwa 20% ya watu wa Umoja wa Ulaya hawaamini uwepo wa roho ya aina yoyote wala miungu, huku Ufaransa na Uswidi zikiongoza kwa idadi kubwa ya waatheisti, zikiunda 40% na 34% kila mmoja.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Tubidy