Uvutano

Taswira ya kani ya uvutano.
Mwendo wa maji yanayotoka kwenye nozeli kuelekea juu unabadilishwa mwelekeo wake kwa umbo la parabola kutokana na kani ya uvutano ya dunia.

Uvutano (pia: mvutano, kani ya mvutano, kanimvutano, nguvu ya uvutano, nguvu mvutano na graviti, kutoka Kiingereza: gravity) ni kani ya kuvutana iliyopo kati ya maada yote ya ulimwengu. Kila gimba lenye tungamo linavuta magimba mengine yote yenye tungamo.

Ndiyo sababu watu wanatembea ardhini ilhali hawawezi kuelea hewani: kwa sababu tungamo ya Dunia inawavuta kuelekea kiini chake. Inavuta kila kitu chenye tungamo kuelekea kiini chake. Sisi watu pia tunaivuta Dunia, lakini kani hiyo ni ndogo mno kulingana na tungamo kubwa ya Dunia. Dunia yetu imeshikwa na uvutano mkali wa Jua na ndiyo sababu ya Dunia kubaki karibu na Jua katika njiamzingo isiweze kwenda mbali.

Uvutano ni kani isiyo na kikomo lakini athira yake inapungua kadiri magimba yalivyo mbali. Unasababisha maada ya anga-nje kupangwa kwa nyota, nebula, majarra na makundi ya majarra.

Isaac Newton anajulikana kama mtaalamu aliyeweza kueleza uvutano kwa mara ya kwanza kama utaratibu wa msingi wa sayansi.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Tubidy